MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA AMEZINDUA WARSHA YA MAFUNZO YA UTOAJI HUDUMA KWA WAGONJWA WA SARATANI

Wananchi wametakiwa kubadilisha utaratibu wa Maisha kwa kutenga muda wa kufanya mazoezi na kula vyakula vyenye Afya ili kupunguza maradhi yasiyoambukiza Nchini ikiwemo Saratani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo katika uzinduzi wa Warsha ya Mafunzo ya utoaji Huduma kwa Wagonjwa wa Saratani iliyofanyika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Ameeleza kuwa Idadi kubwa ya Wagonjwa wa Maradhi ya Saratani inatokana na utaratibu wa Maisha wanayoishi wengi hasa Nchi Maskini zinazoendelea kutokana na kutokuwa na muda wa kufanya mazoezi na kutokula mlo kamili.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inaendelea na ujenzi wa Hospital za Wilaya na Mikoa ambapo ina mpango Maalum wa kuzalisha Wataalamu wa Afya katika Fani mbali mbali kwa lengo la kuhakikisha Hospital hizo zinapata Madaktari wa kutosha pamoja na Huduma Bora na za Kisasa.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed amechukua Fursa hiyo kuipongeza Jumuiya ya Saratani ya Oman kwa kuandaa Mafunzo hayo ambapo Juhudi hizo zitaleta Mabadiliko katika Sekta ya Afya hasa utoaji wa Huduma bora kwa Wagonjwa wa Saratani Nchini.

Ameeleza kuwa maamuzi yalochukuliwa na Jumuiya hiyo ni ya kiungwana na kuwataka washiriki wa Mafunzo hayo kuwa makini kipindi chote na hatimae wakawajibike vyema kwa kuwahudumia wazanzibar na watanzania kwa ujumla.

Aidha ameeleza kuwa hatua nyengine zilizochukuliwa na Wizara ikiwemo Kuanzisha Huduma za Mionzi kwa kuwarahisishia Wananchi kupata Huduma hizo pamoja na kuwasomesha Wataalamu wa Huduma nafuu Ndani na Nje ya Nchi.

Kwa Upande wake Kiongozi wa Jumuiya ya Saratani ya Oman Dkt. Wahid Al kharusy ameeleza kuwa Jumuiya yao imeanza kwasaidia Wagonjwa wa Saratani Nchini Oman na kwa sasa imeanza kusaidia Nje ya Oman kwa lengo la kupunguza Maradhi hayo yanayoenea kwa kasi na kueleza kuwa wameamua kuja zanzibar kutokana na uhusiano uliopo.

Loading