Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar aweka jiwe la msingi la Kituo cha Afya cha Mama na Mtoto Kizimkazi Dimbani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka madaktari na wahudumu wa afya nchini kujitahidi kutoa huduma bora kwa jamii ili juhudi za serikali za kusaidiana na wahisani wa maendeleo katika kimarisha huduma za afya ziweze kuleta tija zaidi kwa wananchi.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko Kizimkazi Dimbani mkoa wa Kusini Unguja, alipozungunza baada ya kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Afya cha Mama na Mtoto kilichonegwa na wahisani kutoka Oman ikiwa ni juhudi za serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya Zanzibar.

Mhe. Makamu amesema kwamba kufanya hivyo pia ndio kuonesha kivitendo kuithamini misaada ya maendeleo inayotolewa na wahisani mbali mbali  katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha huduma kwa wananchi wake.

Amefahamisha kwamba afya ya mtoto anayeweza kuwa na makuzi bora na akili imara inaanza katika hatua  ya kuwepo upatikanaji wa huduma na lishe bora kwa mama na kwamba ni muhimu kwa wahudumu wa afya kujitahidi kuendeleza utoaji wa elimu ya afya kwa mama .

Amesema kwamba taifa linahitaji vijana wenye siha na afya  bora inayotokana na mama kuwa na lishe sahihi na kuweza kumnyonyesha ipasavyo mtoto tokea hatua ya awali ya kuzaliwa ili kuijenga misingi ya afya yake kwa mujibu wa taratibu za kitaalamu.

Aidha amesema kwamba ni wajibu wa wananchi na watumishi wa afya kushirikiana katika kuvitunza vituo hivyo vya afya ili viweze kudumu na kutimiza  malengo ya kuleta huduma zenye tija kwa wananchi.

Kwa upande wake waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, amesema kwamba serikali kupitia wizara hiyo inafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huduma za afya kwa jamii nchini zinaimarika ipasavyo ili kuweza kufikia malengo ya dunia.

Amefahamisha kwamba kutokana hatua hiyo serikali pia  ifikapo Januari mwaka 2024, inakusudia kuifanyia matengenezo makubwa hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja mjini Zanzibar ili iweze kuwa na hadhi na kuwa na kiwango cha kisasa cha utolewaji wa huduma nchini.

Naye Mfadhili wa ujenzi wa kituo hicho kilichogarimu zaidi ya shilingi milioni 77 za Tanzania, amesema kwamba hatua hiyo ni mwanzo wa muendeleo wa kuisadia Zanzibar katika upatikanaji wa hudma kwenye sekta hiyo.

Loading