Maadhimisho ya siku ya Ganzi na Usingizi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha wataalamu wa ganzi na usingizi wanawekewa mazingira bora ya utendaji wa kazi zao ili kuendelea kufanyika upasuaji salama katika hospital zote nchini.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla katika Maadhimisho ya siku ya wataalamu wa Gansi na Usingizi duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema Taaluma ya Ganzi na usingizi ni miongoni mwa Taaluma muhimu katika kada ya Afya hivyo Serikali itahakikisha inawawekea mazingira bora wataalmu hao ikowemo kuwapatia maslahi na stahiki zao zote pamoja na fursa za masomo ya ndani na nje ya nchi ili kuwaongezea ari ya utendaji wa kazi zao.

Sambamba na hayo amewataka wataalamu wa Afya kuendelea kutoa huduma kwa kufuata maadili ya kazi zao ikiwemo upendo, huruma na moyo wa kujitolea kwa wagonjwa, na kutoa wito kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya diploma ya uuguzi kuwa tayari kujiunga na kada hio ili kuweza kuwa na wataalamu wengi katika maeneo ya kiutolea huduma.

Nae Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazurui amesema Wizara imejipanga kuimarisha na kuiboresha Taaluma ya Ganzi na Usingizi kwa kuwasomesha na kuwaendeleza kitelimu watendaji  wa kada hio pamoja na kununua vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. 

Waziri Mazurui amesema kada ya Ganzi na Usingizi imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa na madaktari wasaidizi pamoja na uhaba wa vifaa tiba vya kisasa ambapo kwa Zanzibar nzima madakatari bingwa wa Ganzi na usingizi ni wanne(4)  tu ambao hawatoshelezi kulingana na uhitaji wa tiba hio.

Amewataka wanafunzi wanaojiunga na vyuo kuchagua kozi kulingana na soko la ajira na uhitaji wa wataalamu ikiwemo kada ya Ganzi na Usingizi jambo litakalosaidia kupata wataalamu walio  wengi na wabobezi wa kada hio. 

Akisoma Risala katika maadhimisho hayo mtaalamu wa ganzi na usingizi DKT. SABRINA ABDALLA ALI amesema kada ya Usingizi na Ganzi imekosa kutambulika rasmi kama kada nyengine kutokana na kukosa usimamizi madhubuti na mfumo rasmi wa utendaji wa kazi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kuadhimisha siku ya Ganzi na Usingizi ambapo dunia huadhimisha kila ifikapo tarehe 16 ya mwezi wa 10 kila mwaka na kauli mbiu ya Zanzibar ni Ganzi na Usingizi makini kwa upasuaji salama.

Loading