HOSPITALI ya wilaya Kivunge kwa mara ya Kwanza imefanya upasuaji wa kutumia utaalamu wa matundu madogo (laparoscopy)

HOSPITALI ya wilaya Kivunge, mkoa wa Kaskazini Unguja, imefanya upasuaji wa kutumia utaalamu wa matundu madogo (laparoscopy) ambao ni wa kwanza kufanyika hospitalini hapo.

Mkuu timu ya Madaktari ya Kichina, Profesa Jiang Guoqing, aliongoza kumfanyia upasuaji mgonjwa wa maradhi ya ngiri akisaidia na madaktari wazalendo katika hospitali hiyo.

Akizungumza baada ya upasuaji huo, Profesa Guoqing, alisema, ulikwenda vizuri kutokana na vifaa vya kisasa viliopo hapo huku akiwataka wananchi wa mkoa wa Kaskazini kutumia huduma mbali za matibabu zinazopatika hospitalini hapo.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua inazozichukuwa katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana mijini na vijijini.

Aidha, alisema, timu hiyo ya madaktari wa China inajivunia ushirikiano inaoendelea kuupata kutoka Wizara ya Afya kwenye kuwapatia huduma wananchi.

Msaidizi Daktari Dhamana Hospitali ya wilaya Kivunge, Tamim Hamad Said, alisema, ni mara ya kwanza kwa upasuaji wa aina hiyo na kwa asilimia kubwa umefanikiwa.

Alisema, upasuaji huo ni uthibitisho namna serikali inavyoendelea kuimarisha huduma muhimu za afya kwenye maeneo yote mijini na vijijini.

Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kutumia huduma zinazotolewa hospitalini hapo, ikizingatiwa uwepo wa vifaa vya kisasa vya huduma za afya.

Aidha, alisema, matibabu ya aina hiyo ya upasuaji wa matundu madogo itaendelea kuwa endelevu kwa wananchi watakaokuwa wakiihitaji.

“Miongoni mwa maradhi yanayofanyiwa upasuaji huo ni ugonjwa wa ngiri maji, apendex, uvimbe wa magonjwa ya tumbo na maradhi mengine ya binaadamu.

“Tumeanza kutoa huduma hizi baada ya kugundua kuwa wagonjwa wengi wanabakia majumbani na maradhi kutokana na kuepuka usumbufu wa kwenda na kurudi hospitali ya rufaa Mnazimmoja kufanyiwa upasuaji”, alisema, Dk. Tamimu.

Loading