BARAZA la Tiba Asili na Tiba Mbadala limetakiwa kudhibiti na kusimamia watoaji wa huduma ya Tiba asili na Tiba mbadala

BARAZA la Tiba Asili na Tiba Mbadala limetakiwa kudhibiti na kusimamia watoaji wa huduma ya Tiba asili na Tiba mbadala hapa   nchini ili ziendane na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kuweza kuondokana na matatizo mbali mbali kwa watumiaji wa huduma hizo.

Akizundua Baraza la tano la Tiba Asili na Tiba Mbadala huko Wizara ya Afya Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema nchi mbali mbali zimeweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika tasnia ya tiba asili kwa kutoa mchango mkubwa kwa Serikali kupitia sekta ya afya na kuweza kuwasaidia watumiaji wa tiba hizo.

Aidha amelitaka Baraza hilo jipya lifanye kazi zake kwa uweledi mkubwa sambamba na kukabiliana na wimbi la wadanganyifu wanaozurura kwenye masoko, sehemu za ibada na maeneo mbali mbali kwa lengo la kutapeli na kupotosha wananchi kwa kisingizio cha tiba asili.

Amefahamisha kuwa uzinduzi huo umekwenda sambamba na mapitio ya Sera ya afya ambayo italeta muamko na muelekeo chanya juu ya namna nzuri na iliyo bora ya udhibiti na usimamizi wa huduma ya tiba asili kuendana na mfumo wa tiba mbadala nchini ambapo huduma hizo zitaimarika.

Amesema katika kukabiliana na watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala Wizara ya Afya kupitia Baraza hilo watahakikisha wanawapatia mafunzo maalum ya utayarishaji wa dawa zao kitaalamu ili dawa ambazo zitakidhi vigezo na viwango vya kiusalama ziweze kusajiliwa na kutambulika hapa nchini na sehemu nyengine.

Amesema kuna baadhi ya maduka wanauza dawa hazina viwango na watu wananunua wanatumia na baadae zinapelekea  matatizo mbali mbali yakiwemo matatizo kwenye mafigo, saratani na madhara mengine.

Kwa uapande wake Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Habib Ali Sharif amesema kwa Zanzibar zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa Zanzibar wanapenda kutumia dawa za tiba asili hivyo baraza litahakikisha linasimamia ili kuondokana na matatizo mbali mbali kwa watumiji wa dawa hizo.

Amesema ili Baraza liweze kufanya kazi zake vizuri linahitaji kupatiwa fedha kwa ajili ya ufuatiliji na uendeshaji wa kazi zao na kuweza kukabiliana na wadanganyifu wanaofanya  tiba asili kwa njia isiyo sahihi ambapo alisema  baraza likiwezeshwa litaweza kutatua changamoto nyingi zinazoikabili Tiba asili na Tiba mbadala.

Loading